Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imesema italipelekea Gereza la Kasulu mkoani Kigoma mashine moja ya kisasa ya kutengeneza mkaa mbadala, ili kuliwezesha gereza hilo kuondokana na njia duni zilizokuwa zikitumika awali kuzalisha mkaa mbadala.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika gereza hilo, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, amesema Serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za kuachana na nishati zisizo salama kwa kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rafiki kwa mazingira.

Amesema utoaji wa mashine hiyo utapunguza changamoto za upatikanaji wa mkaa mbadala kutoka maeneo ya mbali, kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuimarisha uzalishaji wa nishati safi kwa kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Kasulu, Bw. Vitalis Mkali, amesema mashine hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani ya gereza sambamba na kulinda mazingira na kuboresha afya kwa watumiaji wa nishati hiyo.