
Wananchi wa Kata ya Chomachankola iliyopo wilayani Igunga mkoani Tabora, wamekataa uwekwaji wa mradi wa skimu ya umwagiliaji katika eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi, wakidai kuwa eneo hilo wamekuwa wakifanyia matambiko ya kimila.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya huku Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paulo Chacha akitolea maelekezo ya suala hilo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamapuli iliyopo katika Kijiji cha Mwanzugi, wilayani Igunga, wenye gharama ya Bilioni 26.9.
RC Chacha, amesema ikiwa wananchi hao wataendelea kushikilia msimamo wao wa kutojengewa skimu ya umwagiliaji kwa kile wanachodai kuwa eneo linalotakiwa kuwekwa mradi huo ni maalum kwa ajili ya matambiko, serikali itapeleka mradi huo kwenye eneo lingine lenye uhitaji.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mboya ameipongeza serikali kwa kupeleka fedha za ujenzi wa skimu hiyo huku akimtaka mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa muda muafaka na ubora mkubwa kwa masilahi mapana ya jamii.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta tija kwa wananchi kiuchumi kutokana na kuwa na kilimo cha uhakika katika kipindi chote cha mwaka.