Jiji la Los Angeles limebadilisha jina la makutano ya mtaa wa Crenshaw Boulevard na Slauson Avenue kwa jina la marehemu Rapa Nipsey Hussle. Makutano hayo yatapewa jina la “Nipsey Hussle Square” ili kuenzi urithi na kujitolea kwa Nipsey kwa jamii.
Sherehe ya kuwekwa wakfu jina la makutano haya zilianza mapema siku ya Jumamosi. Blacc Sam, kaka yake Hussle na Mkurugenzi Mtendaji wa chapa ya The Marathon, alihudhuria pamoja na viongozi kadhaa wa eneo hilo, akiwemo Rais wa Halmashauri ya Jiji la LA, Marqueece Harris-Dawson, Diwani Heather Hutt na Mbunge wa Jimbo la California Isaac Bryan.
Nipsey Hussle, ambaye jina lake halisi ni Ermias Asghedom, alizaliwa Kusini mwa LA. Mara nyingi alizungumza juu ya maisha yake kukua katika Wilaya ya Crenshaw. Itakumbukwa mwaka 2019 aliuwawa kwa kupigwa risasi nje ya duka lake la nguo, lenye chapa ya Marathon, lililo karibu na makutano ya mtaa wa Crenshaw Boulevard na Slauson Avenue.
Hili ni kubwa kwa familia ya Nipsey Hussle na watu wake wa karibu, na ni upendo mkubwa ulioneshwa na jiji la LA.
