Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Ubalozi wa China nchini na Oasis Financial Services Limited, imeendelea kuimarisha ushirikiano na wafanyabiashara wa China kwa lengo la kuboresha ulipaji wa kodi na kuvutia uwekezaji zaidi nchini.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika leo Machi 23, 2026, Mkurugenzi wa Oasis Financial Services Limited, Stambuli Myovela, amesema kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kushauri makampuni, hususan ya China, kuhusu masuala ya kodi ili kuhakikisha yanafuata sheria za nchi na kulipa kodi stahiki kwa wakati.
Amesema miongoni mwa mambo makubwa yaliyojadiliwa ni jitihada za Serikali katika kurahisisha mifumo ya kodi, ikiwemo matumizi ya mfumo wa kidigitali wa ulipaji kodi ujulikanao kama Hydrax, unaomwezesha mlipakodi kulipa kodi kutoka sehemu yoyote duniani.
Kwa mujibu wa Myovela, hatua hiyo inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza Afrika Mashariki kutumia mfumo wa kisasa wa kidigitali, jambo linaloongeza mvuto kwa wawekezaji wa kimataifa, hususan kutoka China.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa za uwekezaji kutokana na wingi wa rasilimali, nguvu kazi ya Vijana wenye ujuzi, pamoja na mazingira mazuri ya kisiasa na kijiografia yanayovutia wafanyabiashara wengi zaidi kuja kuwekeza.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda, amesema lengo kuu la mkutano huo ni kujenga uelewa na ushirikiano mzuri kati ya TRA na wafanyabiashara wa China ili kuhakikisha wanafanya biashara kwa kuzingatia sheria na kulipa kodi kwa haki.
Amesisitiza kuwa TRA haina mgogoro na makampuni ya China, bali inapinga vitendo vyovyote vya ukwepaji kodi bila kujali kampuni inatoka nchi gani.
Mkutano huo unatarajiwa kufungua milango zaidi ya uwekezaji nchini, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China.
