Watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 wametajwa kuwa wahanga wa magonjwa ya koo na pua, huku wazazi wakitakiwa kuchukua tahadhari na hatua za haraka wanapobaini tatizo hilo.
Akizungumza na Redio Kwizera, daktari bingwa wa magonjwa ya koo, pua na sikio aliyeko kwenye kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia mjini Bukoba, Dkt. Kuhu Selema amesema katika mikoa aliyopita amebaini kuwa watoto wengi wanakumbwa na magonjwa hayo na yanaposhindwa kutibiwa huongeza hatari kiasi cha kufanyiwa upasuaji.
Ameongeza kuwa tangu afike mkoani Kagera amekutana na wagonjwa 140 na kati yao, 19 wanafanyiwa upasuaji huku akibainisha dalili za magonjwa hayo kwa watoto ni pamoja na kukoroma sana, kupumulia mdomo, kushtuka shtuka usiku na kwamba wazazi wanapobaini dalili hizi wazazi wachukue hatua za haraka.
Baadhi ya wazazi katika Manispaa ya Bukoba akiwemo Saad Muhamed na Josephene Josephat wamesema kuwa baadhi yao hawakujua kama kukoroma na kushtuka kwa watoto inaweza kuwa hatari na kwamba huichukulia hali ya kawaida kwa mtoto huku wakiwaomba wataalam wa afya kuwapatia elimu zaidi.