
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewasihi akina Mama wote duniani kuendelea kusimama imara siku zote katika kuhamasisha amani ili kuweza kuwakuza watoto katika mazingira mema na yenye ustawi.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akiwasalimia waumini wa Kanisa Katoliki, la Mtakatifu Petro – Blockhauss Jijini Abidjan nchini Ivory Coast May 25, 2025 aliposhiriki ibada ya siku ya Mama Duniani kanisani hapo.
Akiwa ameambatana na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango, Makamu wa Rais amewapongeza waumini wakatoliki wa kanisa hilo kwa kuendelea kumcha Mungu na kushiriki katika kudumisha amani.
Kwa upande wake Padre Felicien Aguie aliyeongoza Misa hiyo ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani, na hatua mbalimbali ambazo imekuwa ikuchukua katika kutafuta amani barani Afrika.
Amesema Tanzania inatajwa kama nchi nzuri kutoka kwa watu mbalimbali wanaoitembelea.
Makamu wa Rais yupo nchini Ivory Coast, kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mikutano ya mwaka ya Bodi za Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itakayofanyika kuanzia Mei 26 hadi 30, 2025 Jijini Abidjan.