
Serikali imesema haitowavumilia wageni haramu wanaoingia nchini kwa nia ya kuhatarisha amani, na kueleza kuwa watu wa aina hiyo ni wahalifu watakaoshughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 26, 2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri Bashungwa amesema kuwa, licha ya jitihada endelevu za serikali kuvutia wageni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo, hakutakuwa na muhali kwa wageni wachache wenye nia ovu ya kuvuruga amani ya nchi.
Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la Polisi kuimarisha usalama ndani ya jamii na kushikamana kulinda nchi dhidi ya maadui wa ndani na nje.