
Serikali Mkoani Kagera imewataka wavuvi wa dagaa katika ziwa Victoria kutumia nyavu za dagaa zisizozidi upana wa mita 60 na mita 20 kwenda chini pamoja na taa sora zizozidi wati 10 ili kuweza kudhibiti vifo vya mazalia ya samaki ambavyo vimekuwa vijikitokea mara kwa mara wakati wa uvuaji wa dagaa.
Afisa Uvuvi Mkoa wa Kagera Bw. Efrazi Mkama amesema hayo wakati akizungumza na wadau wa Uvuvi Wilayani Muleba na kueleza kuwa awali wavuvi walikuwa wanavua dagaa kwa nyavu zenye urefu wa mita zaidi ya 120 na matokeo yake kuvua mazalia ya samaki badala ya dagaa.
Bw. Mkama amesema kuwa kwa sasa wanaendelea kufanya doria za mara kwa mara ziwani kwa ajili ya kuwachukulia hatua wavuvi ambao wanakaidi maelekezo hayo licha kuwapatia elimu.
Miongoni mwa wavuvi wa Samaki katika Kisiwa cha Bumbire Bw. Winchislaus Balongo amesema kwa sasa samaki aina ya sangara wamepungua kwa kuwa wamekuwa wakuvuliwa wachanga na wavuvi wa dagaa hivyo ameshauri elimu iendelee kutolewa ili na wao waweze kuendelea na shughuli zao kama ilivyokuwa awali.