
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema limemkamata na linaendelea kumhoji Diana Edward Bundala ambaye pia hujitambulisha kwa jina la Mfalme Zumaridi (42) Mkazi wa Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa, ambaye ameyageuza makazi yake kuwa Kanisa.
Taarifa iliyotolewa May 15, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa imesema Zumaridi anatuhumiwa kuendesha shughuli za kidini bila usajili pamoja na kufanya mahubiri kwa Waumini wake kwa sauti ya juu katika eneo hilo ambalo ni makazi ya Watu.
Kamanda Mutafungwa pia amesema Zumaridi anahojiwa kuhusiana na taarifa inayoendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kwenye picha mjongeo (video) akiwa na kundi la Watoto wenye umri mdogo wa jinsia ya kike na kiume akiwaeleza kuwa yeye ndiye Mungu wao ambaye ana uwezo wa kuwatenganisha na kifo
Aidha Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Mwanza amesema Uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea na kubainisha kuwa katika uchunguzi huo litashirikiana na Taasisi nyingine za Serikali
Hata hivyo Jeshi la Polisi linawaomba Wananchi wenye taarifa mbalimbali zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tuhuma hizi wafikishe kwa Jeshi la Polisi, uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zinazostahili zitachukuliwa.