
Serikali ya Tanzania imeanza kuchukua hatua kudhibiti magugumaji katika Ziwa Victoria kwa kutumia mitambo mipya na ya kisasa iliyonunuliwa na serikali.
Hatua hiyo imetangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Mei 19, 2025, wakati wa ziara yake ya kikazi katika eneo la Kigongo-Busisi, mkoani Mwanza, ambako amekagua shughuli za udhibiti wa magugumaji.
Magugumaji hayo yameathiri shughuli muhimu za kijamii na kiuchumi kama vile uvuvi, usafiri na usafirishaji, na yameenea katika eneo la zaidi ya ekari 300 ndani ya ziwa hilo.
Serikali, kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, imeendelea na kazi ya kuyaondoa magugumaji hayo, ambayo yanajumuisha aina tatu: Salvinia molesta (jipya), Water hyacinth, na Lutende.
Kazi ya kuteketeza magugumaji inatarajiwa kukamilika Julai 2025, hatua itakayofungua njia kwa urejeo wa shughuli za kijamii na kiuchumi katika maeneo ya ziwa hilo.