
Rais Samia Suluhu Hassan leo ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wilayani Busega Mkoa wa Simiyu wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 440, ambao utaanza kwa hatua ya kwanza kwa maeneo ya Busega, Itilima na Bariadi na baadae utafika hadi katika wilaya za Maswa na Meatu.
Akitoa maelezo mbele ya Rais Samia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema mradi huo utahudumia wananchi wa vijiji 103, na kwa sasa kazi ya ulazaji wa mabomba inaendelea ili kuwafikia wananchi.
Aidha Rais Samia amewahimiza Watanzania kuchapa kazi kwa bidii na kuongeza uzalishaji ili kuiwezesha nchi kujitegemea kiuchumi na kwamba Serikali ipo kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanapatikana.
Ameongeza kuwa Tanzania imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa la sita kwa ukubwa barani Afrika la JP Maguli lililoko jijini Mwanza, kutokana na Amani na utulivu ukiwamo wa kisiasa.