
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali ambazo hazijajiunga na mfumo wa kielektroni utakaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana (GovESB) kujiunga na mfumo huo ifikapo Julai 30 mwaka huu ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Ametoa maagizo hayo leo Jumatatu (Juni 23, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa mfumo huo unafaida kubwa katika utumishi wa umma kwani utasaidia kurahisisha utendaji, kutoa taarifa kwa wakati, kuondoa makosa ya kibinadamu katika kuwahudumia wananchi pamoja na kuwabana wala rushwa.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zihakikishe mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo wa GovESB ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea kuboresha huduma za Serikali.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia miiko na maadili ya utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingitia Sera na Sheria kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema Tanzania imetambulika kimataifa ambapo mwaka 2022 Benki ya Dunia ilifanya utafiti kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Amefafanua kuwa ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Machi, 2023 ilibanisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 duniani, nafasi ya 2 Afrika na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.
Katika tukio hilo, Mheshimiwa Majaliwa alizindua mifumo miwili ambayo ni Mfumo wa kielektroni unaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GovESB) Pamoja na Mfumo wa e-Wekeza unaomuwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).
Siku ya Utumishi wa Umma husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.