
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam, Ho Duc Phoc, pembezoni mwa Mkutano wa Nne wa Kimataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) unaofanyika Sevilla, Uhispania.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mpango amepongeza ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Vietnam, ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 60. Amesema Vietnam ni moja ya nchi za mwanzo kufungua ubalozi nchini Tanzania na kushirikiana kwa karibu kupitia Serikali, chama na wananchi.
Makamu wa Rais amesema Tanzania itaendeleza ushirikiano huo, hususan katika uwekezaji, biashara, kilimo, ulinzi na masuala ya kikanda na kimataifa aidha ameikaribisha Vietnam kuchangamkia fursa mbalimbali za uwekezaji nchini na kuahidi kuitisha Tume ya Pili ya Ushirikiano wa Pamoja baada ya uchaguzi wa 2025.
Kwa upande wake, Ho Duc Phoc ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano imara na kufichua kuwa mauzo ya bidhaa kati ya nchi hizo hufikia dola milioni 150 kwa mwaka. Amehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano huo kupitia mashirika ya biashara na uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango amekutana na Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Elsebeth Søndergaard Krone, na kuzungumzia kuimarisha ushirikiano katika nishati, miundombinu, kilimo janja, na uwezeshaji wa sekta binafsi.
Makamu wa Rais pia amehudhuria mkutano wa nchi zinazoendelea ulioongozwa na Waziri Mkuu wa Nepal, uliolenga kuendeleza jitihada za ndani za mapato na utekelezaji wa azimio la Doha la 2023.