
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeahidi kuendelea kuwa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na pia kuwa na usimamizi unaozingatia matakwa ya utawala bora.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Khatib Mwinyichande ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam na kuongeza kuwa tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewapatia kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi huo.
Amesema tume hiyo imekuwa ikifuatilia mchakato mzima wa uandikishaji wapiga kura, na itafuatilia kampeni pamoja uchaguzi mwezi Oktoba.
Kamishna Mwinyichande pia amesema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaendelea kupokea na kuyapatia ufumbuzi matatizo na kero mbalimbali za wananchi.