
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wafugaji mkoani humo kuitikia zoezi la uchanjaji wa mifugo linaloendelea nchini kote ili wanufaike na mifugo yao.
Balozi Sirro ametoa wito huo akiwa wilayani Uvinza kushuhudia utekelezaji wa Kampeni ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo mkoani Kigoma ambapo ng’ombe 800 na kuku 100 wamefikiwa.
Aidha Balozi Sirro amesema Matatizo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe yatamalizika endapo wafugaji watazingatia na kushiriki katika zoezi hili la chanjo kikamilifu ambapo takribani mifugo 300,000 inatarajiwa kuchanjwa mkoani Kigoma.
Akizungumza Kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene amesema zoezi hilo limeanza vizuri mkoani Kigoma ambapo limeanza kwa kutibu magonjwa manne ambayo ni homa ya mapafu kwa ng’ombe na homa ya mafua.