
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ameishukuru serikali kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye eneo la ziwa victoria ili kuhakikisha wananchi wake wanakua salama wanaposafiri na kufanya shughuli za uvuvi.
Mtanda amebainisha hayo leo julai 07, 2025 mara baada ya kukagua Meli ya Kisasa ya Uokozi na Matibabu iliyojengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 4.5 chini ya mradi wa Kikanda wa Usafiri na Mawasiliano Ziwa Victoria unaojumuisha nchi ya Tanzania na Uganda.
Aidha, amesema boti hiyo ya kisasa italeta fursa kwa wagonjwa watakaopata dharula zozote ndani ya maji, boti hiyo itawafikia kwa haraka na kutoa Matibabu ya dharura kabla ya kufikishwa nchi kavu kwa ajili ya kupelekwa hospitali ya rufaa katika eneo husika.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza ameongeza kuwa moja ya mambo yaliyo chini ya mradi huo ni pamoja na kuweka mawasiliano na kujenga kituo cha Kikanda cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji kilichopo Ilemela na ununuzi wa boti hii pamoja na boti mbili ndogo za utafutaji na uokoaji.
Naye Afisa Mfawidhi Mkoa wa Mwanza kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Joseph Mkumbo amesema boti hiyo ya kisasa ina uwezo wa kutembea maili 18 kwa saa.
Aidha, amebainisha kuwa imewasili mkoani Mwanza kutoka bandari ya Mtwara tarehe 23 Juni, 2025 na kwamba kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza walifanikisha kuishusha majini tarehe 05 Julai 2025 kwenye bandari ya Mwanza Kusini.
Ameongeza kuwa tayari TASAC wameifanyia majaribio majini na kuonesha mafanikio makubwa sana kwani imetumia muda wa saa 1 kwenda Ukerewe tofauti na meli zinazotumia masaa 3 hadi 4 na ameongeza kuwa mradi huo unahusisha pia ununuzi wa boti mbili zingine zenye vifaa.