
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) nchini, Crispin Chalamila ameeleza kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa kwa ustawi wa wananchi, na inachangia kuwepo kwa vitendo vingine vya kidhalimu ambavyo vimekatazwa katika Katiba ya Tanzania.
Chalamila ameyasema hayo leo jijini Dodoma, katika maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa barani Afrika.
Amesema jitihada za kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa zitachangia kufikia lengo la Serikali la kuleta ustawi wa jamii ya Watanzania na kukuza heshima ya ubinadamu.
Ameongeza kuwa majadiliano kuhusu rushwa yanayofanyika katika maadhimisho hayo yatasaidia kukuza heshima ya binadamu barani Afrika, ambao mara nyingi huchukuliwa haki zao kutokana na vitendo vya rushwa.
Naye mwakilishi wa Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Rushwa ya Umoja wa Afrika, Benjamin Kapera, amesema kwa mujibu wa Mfuko wa Mo Ibrahim, Afrika inapoteza takribani dola bilioni 128 za Kimarekani kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa, sawa na asilimia 50 ya mapato yake ya kodi na asilimia 25 ya pato la Taifa.