
Watoto wawili mapacha wa familia moja wamefariki baada ya nyumba waliyokuwemo kuteketea kwa moto katika Kitongoji cha Nyakiziba Kijiji cha Kakoma Kata ya Burungura Wilayani Muleba Mkoani Kagera.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyakiziba Bw. Godwin Felecian amewataja watoto hao kuwa ni Maria Jovine na Zakaria Jovine wenye umri wa miezi mitano, na kwamba tukio hilo limetokea Augost tisa mwaka huu, baada ya mama yao mzazi kuwaacha ndani wakati chakula kikiwa jikoni na aliporejea akakuta watoto hao wameteketea kwa moto.
Bw. Godwin amesema kuwa baada ya kutokea tukio hilo uongozi wa Kitongoji hicho ulitoa taarifa jeshi la Polisi na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati wakiwa wanapika hasa nyumba ambazo zimeezekwa kwa nyasi.
Aidha jeshi la Polisi Wilayani humo limefika eneo la tukio likiambatana na Mganga mafawidhi wa zahanati ya Kishuro kwa ajili ya uchunguzi wa miili hiyo na kuruhusu tataratibu za mazishi ziendele.