
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuenzi mema yote yaliyofanywa na hayati Ndugai enzi za uhai wake, akisema mchango wake katika uongozi wa Bunge na Taifa utabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo.
Majaliwa ameyasema hayo leo Agosti 11, 2025 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, yaliyofanyika shambani kwake, kijiji cha Msunjulile, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Akizungumza katika ibada ya mazishi, Majaliwa amesema kuwa akiwa mwakilishi wa wananchi wa Kongwa, hayati Ndugai ametoa mchango mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake.
Amesema hayati Ndugai alikuwa mlinzi wa taratibu za Bunge na mshirika wa karibu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na Serikali kwa masilahi mapana ya Taifa, akisisitiza mawasiliano ya uwazi, mshikamano na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa ajenda za kitaifa.