
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia walimu kuwa Serikali itaendelea kuimarisha maslahi na mazingira ya ufundishaji na kujifunza kwa dhamira ya kuboresha elimu zaidi.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 12 Agosti 2025, katika kongamano na Shirikisho la Walimu Zanzibar ikiwa sehemu ya kumpongeza Rais Mwinyi kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu katika kipindi cha uongozi wake.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, katika kuongeza motisha kwa walimu, Serikali imeboresha maslahi yao kwa kuongeza mishahara, posho za likizo na ufiwa, pamoja na kulipa malimbikizo mengine.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeajiri walimu wapya 5,265 na kuwapatia mafunzo mbalimbali ili kuongeza ufanisi wao.
Ameeleza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kimetumika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa malipo ya rambirambi kwa wafiwa, pamoja na posho za walimu wakuu na wasaidizi, ikiwemo nyongeza ya posho za madaraka.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali imeamua kukirejesha Chuo cha Ualimu cha Nkrumah kufuatia ombi la walimu, kutokana na kazi nzuri iliyokuwa ikifanywa na chuo hicho, ili kiendelee kuzalisha walimu bora na wenye sifa za ufundishaji. Vilevile, Serikali imeanzisha Tume ya Walimu itakayoshughulikia changamoto zinazowakabili walimu.