
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amemcharukia mkandarasi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu Dodoma, akimtaka kufidia muda uliopotea.
Dk Biteko ambaye ametembelea kukagua utekelezaji wa mradi huo leo Agosti 20, 2025 , ameeleza kutoridhishwa na kasi ya mradi huo ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31, lakini kwa sasa upo asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba mwaka 2024.
Kuchelewa kwa mradi huo kumebainika baada ya Dk Biteko kukagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino, Dodoma na hapo akamtaka mkandarasi Kampuni ya TBEA ya China kufidia muda wa kazi uliopotezwa wa asilimia saba ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.
Novemba, 2024 Serikali ilikubaliana na mkandarasi huyo kutekeleza mradi huo ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwani, wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.