
Baada ya kuandika barua ya wazi kwa waandaaji wa CHAN2024 iliyofanyika 2025, msanii wa Bongo Fleva Zuchu sasa amethibitisha kulipwa malipo yake yaliyokuwa yamecheleweshwa.
Mwanzo, Zuchu alieleza kusikitishwa na hatua ya wakala wa tamasha hilo, LEAP Creative Agency, kushindwa kumlipa kwa mujibu wa makubaliano baada ya kutumbuiza kwenye fainali jijini Nairobi, Agosti 30, 2025.
Kupitia barua hiyo, alidai kupokea nyaraka za malipo (POPs) ambazo hazikuwa halali na akaonya kuchukua hatua zaidi iwapo malipo hayangekamilika.
Hata hivyo, siku chache baada ya barua hiyo kusambaa, Zuchu kupitia instastory yake alithibitisha kuwa amepokea malipo yake yote.
“Nataka kuwashukuru watu wangu wema waliowezesha ujumbe wetu kufika kwa wakala aliyehusika na CHAN. NIMEPOKEA MALIPO YANGU YOTE, ASANTENI. SASA TUNASONGA MBELE,” aliandika Zuchu kupitia InstaStory.
Tukio hili limemulika uwajibikaji wa waandaaji wa matamasha makubwa barani na umuhimu wa kuheshimu kazi ya wasanii wanaotoa mchango wao katika burudani na tasnia ya muziki.