
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimepiga hatua kubwa katika matumizi ya rasilimali za ndani na uwekezaji katika sekta ya elimu kwa maendeleo endelevu.
Ametoa kauli hiyo leo, Septemba 24, 2025 mkoani Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa kongamano la tano la kimataifa la Elimu Bora, likiwa na kauli mbiu “Kuimarisha mifumo na uwekezaji: Kusonga mbele katika Uhamasishaji wa Rasilimali za Ndani kwa ajili ya Elimu Jumuishi, Bora na Endelevu Barani Afrika”.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa hatua zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kutunga na kuboresha sera, sheria, na miongozo mbalimbali ya elimu, pamoja na kuongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi trilioni 4.72 katika mwaka wa fedha 2020/2021 hadi shilingi trilioni 6.16 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, amefafanua kuwa ongezeko hilo la bajeti limeimarisha mazingira na miundombinu ya elimu kwa maendeleo endelevu.
Pia, Serikali imeongeza wigo wa Sera ya Elimu Bila Malipo kwa elimu ya Sekondari, ambapo mwaka 2020 ilitengwa shilingi bilioni 312.08 na mwaka 2024 ilitengwa shilingi bilioni 796.58, ikiwa ni ongezeko la shilingi bilioni 484.
“Ongezeko hili limepunguza changamoto za kifedha zinazokwamisha sekta ya elimu na kuongeza idadi ya wanufaika kutoka wanafunzi 14,940,925 mwaka 2020 hadi 16,155,282 mwaka 2024,” ameeleza Dkt. Biteko.
Amewahimiza washiriki wa kongamano hilo kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ili kufikia utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya kuelekeza asilimia 20 ya bajeti ya nchi katika maendeleo ya sekta ya elimu