
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua dawati maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi wilayani Kahama mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara kurasimisha biashara zao, kupata elimu ya kodi na huduma bora kutoka katika mamlaka hiyo.
Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya ofisi za TRA Kahama na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wawakilishi wa wafanyabiashara Wilayani humo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa TRA Mkoa wa Kikodi Kahama, Siwaka Kamwamu, amesema dawati hilo litakuwa kiungo muhimu kati ya TRA na wafanyabiashara wadogo kwa kuwasaidia kusajili biashara zao, kuelewa wajibu wao wa kikodi na kupata huduma kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kahama, Charles Machali, Ameahidi kushirikiana na TRA kwa kulipa kodi kwa hiari ili kujenga mazingira bora ya biashara na uchumi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, ameeleza kuwa uzinduzi wa dawati hilo ni utekelezaji wa agizo la serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha kila mfanyabiashara anatambuliwa na kushirikishwa katika maendeleo ya taifa.