
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, amesema taaluma ya uhandisi moyo wa taifa kwani Taifa haliwezi kupiga hatua za haraka za maendeleo bila kuwekeza kwa dhati katika taaluma ya uhandisi huku akisisitiza kuwa sekta hiyo ni injini ya ukuaji wa viwanda na maendeleo ya teknolojia.
Akizungumza leo Septemba 25, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa akifungua wa Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi, alipomwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Dkt. Biteko alibainisha kuwa tafiti zinaonesha kila dola moja inayowekezwa katika uhandisi huzalisha kati ya dola saba hadi kumi.
Amesema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wabunifu wapya katika teknolojia duniani wanatokana na taaluma ya uhandisi, huku akiitaja sekta ya nishati na akili bandia kama mifano ya maeneo yanayoongozwa na wahandisi. Aidha, ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maendeleo ya viwanda yanategemea huduma za moja kwa moja kutoka kwa wahandisi.
Aidha Dk. Biteko ametoa wito kwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuwajali na kuwawezesha wahandisi vijana, badala ya kuwadidimiza, ili nao waweze kukua kitaaluma na kushika nafasi za usimamizi wa miradi mikubwa siku za usoni.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza ERB kuhakikisha inatoa motisha kwa wahandisi wanaotekeleza miradi kwa ubora wa hali ya juu, kwa lengo la kuongeza ushindani wa kitaaluma na kuchochea bidii kazini.
Kwa upande wake waziri wa Ujezi Abdallah Ulega amesema wizara itaendelea kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazawa katika kutekeleza miradi ya mikubwa ya kimaendeleo kama ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere lakini ujenzi wa reli ya SGR.
Naye, Kaimu msajili ERB Mercy Jilalala amesema kufutia jitihada mbalimbali zinazofanywa na bodi hiyo zimepelekea mabadiliko makubwa katika sekta ya uhandisi nchini ambapo maazimisho ya mwaka huu yamekutanisha washiriki zaidi ya 4000 ambao wameshiriki moja kwa moja lakini zaidi ya washiriki 700 wameshiriki kwa njia ya mtandao.
Maazimisho ya 22 ya siku ya wahandisi yenye kauli mbiu isemayo ‘wajibu wa wahandisi kuelekea dira ya maendeleo 2050’ yameenda sambamba na uzinduzi wa Application mpya iitwayo ERB mwandisi App ambayo itawasidia wananchi kujua ni wahandisi gani wanaweza kuwatumia kutokana na shughuli zao kwani kupitia app hiyo watajua wahandisi waliosajiliwa.