
Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Loveness Kisile (30), mkazi wa Mtaa wa Temeke, jijini Mwanza akituhumiwa kutoa taarifa za uongo kwa askari, ndugu, jamaa na marafiki kuwa ametekwa.
Anadaiwa kutoa taarifa kwa mume na ndugu zake kwamba ametekwa na watu watatu waliotaka Sh10 milioni ili wasimdhuru na kuondoa ujauzito aliokuwa nao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo Septemba 24, 2025 saa 5:30 usiku, baada kumpigia simu mume wake, Hosea Lusingwa akidai watu hao walimkamata kwa nguvu, kumfunika uso na kumpeleka kusikojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Septemba 25, 2025 Kamanda Mutafungwa amesema taarifa hizo zilizua taharuki kwa mume na ndugu na kulihangaisha Jeshi la Polisi usiku kucha, kwani awali Loveness alimweleza mume wake kwamba ni mjamzito wa pacha watatu.
Amesema mume alitoa taarifa Kituo cha Polisi Nyakato akidai watekaji wanahitaji Sh10 milioni na kama asingefanya hivyo wangemchoma mke wake sindano ya kutoa mimba.
”Baada ya muda mfupi alimjulisha mume wake kuwa mimba imetolewa na watoto wake pacha watatu wamefariki dunia, akisisitiza atume kiasi hicho cha fedha ili aachiwe huru,” amesema.