
Tanzania imefanya majadiliano na nchi ya Hungary ili kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Biharamulo mkoani Kagera.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahomud Thabit Kombo, ameongoza majadiliano hayo yaliyohusu mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Hungary kwa lengo la kutekeleza mradi huo wa usambazaji maji.
Majadiliano hayo yamefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar es Salaam kati ya Serikali ya Tanzania na ujumbe kutoka Serikali ya Hungary, ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa nchi hiyo, Péter Szijjártó.
Balozi Kombo amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha jamii inaondokana na uhaba wa huduma ya maji safi na salama.
Amesema mradi huo unatarajiwa kutumia teknolojia za kisasa kusafirisha maji kutoka Ziwa Victoria na kuyatibu kabla ya kuwafikishia wananchi.
Naye Waziri Péter Szijjártó amesema Serikali ya Tanzania imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo na Hungary, akieleza kuwa uhusiano huo umewezesha kuanzishwa kwa mradi huo wa masharti nafuu kwa usalama wa afya ya wananchi na Afrika kwa ujumla.
Ziara ya Waziri Szijjártó na majadiliano kuhusu sekta ya maji yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya Tanzania na Hungary.
Katika hatua nyingine Waziri Balozi Kombo ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Hungary kwa uamuzi wake wa kufungua Ofisi ya Dar es Salaam ya Ubalozi wa Hungary na kuitaja hatua hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili.
Amesema kuwa, ufunguzi wa Ofisi hizo ambazo zipo Masaki jijini Dar es Salaam ni heshima na upendeleo kwa Tanzania ambayo inadhihirisha namna ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ulivyoimarika na kwamba hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara, uwekezaji, utalii, mahusiano baina ya wananchi wa mataifa haya mawili na huduma nyingine za kidiplomasia na kikonseli zitakazotolewa na Ubalozi huo.