
Serikali imetangaza mkakati wa kuimarisha mifumo ya kutatua migogoro ya ndoa kupitia usuluhishi, kwa kuboresha utendaji wa bodi za usuluhishi na kuwajengea uwezo wasimamizi pamoja na wajumbe wake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, akifungua kikao cha bodi hizo jijini Arusha September 29, 2025, amesema familia ndiyo msingi wa malezi, maadili na ustawi wa jamii, na kwamba migogoro ya ndoa mara nyingine kuwaacha watoto wakihangaika na kuongeza idadi ya watoto wa mtaani.
Maswi amesema Takwimu zinaonesha, mwaka 2021 kulikuwa na talaka 523, mwaka 2022 talaka 447, mwaka 2023 talaka 711, na mwaka 2024 talaka 1,569 zilisajiliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kwa Umma, Angela Anatory, amesema usuluhishi husaidia wanandoa kuelewana na kuondoa uhasama, hivyo kupunguza kuvunjika kwa ndoa.