
Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Vincent Cosmas Mwagala, ameeleza kuwa Padri Jordan Kibiki hakutekwa kama ilivyoripotiwa awali, bali alikumbwa na hali ya unyongefu (depression) kutokana na hasara aliyopata kwenye biashara ya mtandaoni.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa leo, Askofu Mwagala amesema Kibiki aliingia kwenye msongo wa mawazo baada ya kugundua kuwa amepoteza takribani Shilingi milioni 3.5 katika mtandao wa eBay.
Amefafanua kuwa kati ya fedha alizopoteza, Shilingi 500,000 alikuwa ameazima kwa Paroko na Shilingi milioni 1.5 kwa mhasibu wa jimbo, na kwamba kiasi kilichosalia kilitokana na fedha zake mwenyewe, hivyo hakukuwa na madeni makubwa ya kumfanya kujiingiza katika vitendo vya hatari.
Awali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kupitia Kamanda Allan Bukumbi lilieleza kuwa baada ya uchunguzi, Kibiki alikutwa Mbalizi mkoani Mbeya na hakuwa ametekwa kama alivyodai kupitia mtandao wa WhatsApp.
Aidha Askofu amesema kwa mujibu wa sheria za kanisa, jinai au madai yanayomhusu Padre binafsi, si ya kanisa bali ni yake yeye mwenyewe, hata hivyo ni wajibu wa kanisa kutafuta ukweli wa tuhuma bila kuingilia kazi za vyombo vya uchunguzi kama walivyofanya katika tukio hilo.