
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano nchini kimeshuka kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.
Majaliwa amesema hayo, Septembe 30, 2025 wakati akifunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa, kiwango cha ukondefu miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano nacho kimepungua kutoka asilimia 5 mwaka 1992 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.
Amesema kuwa Serikali inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii na kwamba lengo ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora
Kadhalika, Majaliwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa kinara wa mapambano dhidi ya utapiamlo kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele kwa kuimarisha bajeti, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na uhamasishaji wa afua za lishe kuanzia ngazi ya Taifa hadi vijijini.
“Jitihada hizi zilimuwezesha kupata tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates Foundation, kutokana na mchango wake mkubwa katika kusukuma mbele Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan kwenye afya ya mama, mtoto na lishe,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.