
Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limewataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mikononi, na badala yake watoe taarifa za matukio ya uhalifu kwa Jeshi la Polisi au vyombo vingine vya dola.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 30, 2025, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mauaji ya vijana wawili lililotokea katika mtaa wa Igelegele, kata ya Mahina, wilaya ya Nyamagana.
Kwa mujibu wa Kamanda Mtafungwa, vijana hao walidaiwa kuwa wahalifu walivamiwa na kundi la wananchi waliokuwa na hasira kali, ambao waliamua kuwashambulia badala ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Jeshi la Polisi liliwasili katika eneo la tukio na kufanikiwa kuwatoa mikononi mwa wananchi hao.
Hata hivyo, vijana hao wawili walikuwa tayari katika hali mbaya na walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando kwa matibabu ya dharura.
Licha ya juhudi za kitabibu, majeruhi hao walifariki dunia usiku huo wa tarehe 26 Septemba 2025, wakiwa wanaendelea na matibabu katika hospitali hiyo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Bugando kwa ajili ya uchunguzi zaidi, ambapo taratibu za Uchunguzi zinaendelea kabla ya miili hiyo kukabidhiwa kwa familia zao kwa mazishi.
Kamanda Mtafungwa amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na linawasaka watu wote walioshiriki katika kitendo hicho na ameeleza wazi kuwa kujichukulia sheria mikononi ni kosa la jinai na yeyote atakayebainika atafikishwa mahakamani mara moja.
“Tunaendelea kuwasaka watuhumiwa wote. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote aliyejihusisha na tukio hili,” alisema Mtafungwa.
Jeshi la Polisi pia linatoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kwa wakati kuhusu matukio ya uhalifu, ili vyombo vya usalama viweze kuchukua hatua stahiki bila kuhatarisha maisha ya watuhumiwa au usalama wa jamii kwa ujumla.