
Bei za petroli, dizeli, na mafuta ya taa kwa mwezi Oktoba 2025 zimeendelea kushuka, ambapo bei za rejareja za petroli zimepungua kwa shilingi 55, na dizeli kwa shilingi 50, ikiwa ni mwendelezo wa kupungua kwa bei za bidhaa hizo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile imeeleza kuwa kupungua kwa bei hizo kumetokana na kushuka kwa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa wastani wa asilimia 5.10, pamoja na kupungua kwa gharama za kuagiza mafuta ya petroli kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani wa asilimia 1.95.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya mafuta yaliyopokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam imepungua kutoka shilingi 2,807 hadi 2,752 kwa petroli, na kutoka shilingi 2,754 hadi 2,704 kwa dizeli, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki kuwa shilingi 2,774 kama ilivyokuwa mwezi Septemba 2025.
Kwa mafuta ya petroli yaliyopokelewa katika Bandari ya Tanga, bei ya rejareja pia imepungua kutoka shilingi 2,868 hadi 2,813, dizeli kutoka shilingi 2,816 hadi 2,766, na bei ya mafuta ya taa imesalia kuwa shilingi 2,835 kama ilivyokuwa mwezi uliopita.
Kwa mafuta yanayopokelewa Bandari ya Mtwara, bei ya petroli imepungua kutoka shilingi 2,899 hadi 2,844, na dizeli kutoka shilingi 2,847 hadi 2,797, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki kuwa shilingi 2,866 kama ilivyokuwa mwezi Septemba 2025