
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ametembelea ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama na kuagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi huo, ili kukamilisha mradi kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
Akizungumza mara baada ya kukagua hatua za utekelezaji wa mradi huo, Mhita amesema kuwa ujenzi huo ni mradi wa kimkakati kwa mkoa wa Shinyanga wenye lengo mahsusi la kuokoa maisha ya mama na mtoto, hivyo kasi ya ujenzi ni lazima iendane na uwekaji wa fedha.
“Kasi ya ujenzi iongezeke! Suma JKT ambao ndio wakandarasi wa mradi huu muongeze bidii ili jengo likamilike mapema. Fedha inayowekwa ni nyingi, ni lazima ionekane kwenye hatua za ujenzi,” alisisitiza Mhita.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ambapo tayari kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 kimelipwa.
Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 75 badala ya asilimia 80 iliyotarajiwa kufikiwa kwa hatua ya sasa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu, ameeleza kuwa fedha za kumalizia ujenzi huo zipo tayari, lakini zitatolewa kulingana na kasi na ubora wa kazi unaoendana na fedha zilizolipwa awali.
Kwa upande wake, Mhandisi wa mradi kutoka SUMA JKT, Bw. James Simon amesema wapo tayari kuongeza kasi ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa kufikia Januari 2026 kama mkataba unavyobainisha.
Mhita amesisitiza kuwa atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo hadi utakapokamilika, ili kuhakikisha wananchi wa Kahama na mkoa mzima wa Shinyanga wanapata huduma bora za afya, hasa akina mama na watoto.
Mpaka kukamilika kwa jengo hilo zaidi ya bilioni 6.8 zitatumika kukamilisha jengo hilo linalotazamiwa kuwa mkombozi wa kupunguza Vifo vitokanavyo na Mama na Mtoto.