
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kufanikisha makusanyo ya kodi ya jumla ya Shilingi Trilioni 8.97 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26 (Julai–Septemba 2025), ikiwa ni sawa na asilimia 106.3 ya lengo la Shilingi Trilioni 8.44.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 2, 2025 jijini Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, makusanyo hayo yameonesha ukuaji wa asilimia 15.1 ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 7.79 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, makusanyo hayo yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 104 ukilinganisha na Shilingi Trilioni 4.40 zilizokusanywa katika robo hiyo hiyo mwaka 2020/21 wakati Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilipoingia madarakani.
Wastani wa makusanyo ya kila mwezi pia umeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.47 mwaka 2021/22 hadi Shilingi Trilioni 2.99 mwaka 2025/26, huku mwezi Septemba 2025 ukivunja rekodi kwa makusanyo ya Shilingi Trilioni 3.47.
“Kipekee, kwa mara ya kwanza Mamlaka ya Mapato Tanzania imeweza kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 3.47 kwa mwezi mmoja wa tisa ambacho ni kiasi kikubwa kuliko miezi mingine ya nyuma kama hiyo”, imeeleza taarifa ya TRA
TRA imesema ufanisi huo umechangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo kuimarika kwa mahusiano na walipakodi na kuhamasishwa ulipaji wa hiari bila uonevu, kuongezeka kwa uwajibikaji wa walipakodi na shughuli za kiuchumi kutokana na sera bora za Serikali, uboreshaji wa mazingira ya biashara kupitia uanzishwaji wa Dawati la Uwezeshaji Biashara nchi nzima, muitikio mzuri wa wafanyabiashara wa mtandaoni kwenye kampeni za usajili na ulipaji kodi, hasa sekta ya malazi na usimamizi madhubuti wa mifumo ya kodi, ikiwemo TANCIS, matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs), na mifumo ya Tehama ya ndani.
Pamoja na kuendelea kutoa elimu ya kodi, TRA imeanzisha huduma mbalimbali kwa walipakodi ikiwemo:
ofisi kufunguliwa Jumamosi na Jumapili, siku maalum za “Kusikiliza Walipakodi” kila Alhamisi, na programu ya Mabalozi wa Kodi ili kusikiliza na kutatua changamoto.