
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kuzingatia usimamizi mzuri wa fedha binafsi kwa kuweka akiba, kuepuka madeni yasiyo ya lazima, na kuishi kwa kuzingatia kipato chao ili kujenga msingi imara wa maendeleo binafsi na ya familia.
Mtanda ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo ya elimu ya fedha iliyofanyika jijini Mwanza iliandaliwa na Chuo cha Mafunzo Benki Kuu ya Tanzania ikiwa na lengo la kuwajengea Viongozi wa Taasisi za dini na Kamati ya Usalama Mkoa uelewa kuhusu masuala ya kifedha, hususan namna ya kupanga matumizi, kuweka akiba, na kujiepusha na madeni ambayo yamekuwa chanzo cha migogoro ya kifamilia na hata umaskini wa muda mrefu.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema watu wengi wamejikuta wakikopa ili kufanikisha matumizi ya anasa, badala ya kuwekeza au kuweka akiba kwa ajili ya dharura.
“Tunapaswa kujifunza kuishi ndani ya uwezo wetu na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima”.
Aidha, Mhe. Mtanda amewaasa Viongozi hao na wale wanaowaogoza kuanzisha utaratibu wa kuweka akiba kila mwezi, hata kama ni kiasi kidogo, akibainisha kuwa nidhamu ya kifedha inaanza na maamuzi madogo ya kila siku.
Mkuu huyo wa Mkoa ameongoza kuwa madeni yasiyo na tija yamekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya watu wengi. Alitoa mfano wa watu wanaokopa kwa ajili ya sherehe au mitindo ya maisha, badala ya kuwekeza katika elimu, afya au biashara.
Semina hiyo imehudhuriwa na zaidi ya watu 200 kutoka Taasisi mbalimbali za Dini lakini pia wakiwemo Viongozi wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Mwanza ambao wamepata fursa ya kuuliza maswali na kushiriki mijadala kuhusu changamoto za kifedha zinazowakabili.