
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewahakikishia Watanzania kuwa litaendelea kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika mamlaka husika za haki jinai wote wanaotumia mitandao ya kijamii kutengeneza, kuandika au kusambaza maandishi na picha zenye mwelekeo wa kuchochea vitendo vya kihalifu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumapili, Oktoba 5, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, watu hao wamekuwa wakifanya vitendo vinavyokiuka maadili ya Mtanzania, utamaduni wa Taifa na sheria za nchi, huku wakisababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi wema.
“Vitendo hivi vinasukumwa na dhamira ovu na vimekuwa vikisababisha hofu kwa wananchi wengi. Jeshi la Polisi linaendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa linaendelea kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika mamlaka nyingine za haki jinai kwa hatua za kisheria kama ambavyo limeshafanya kwa waliokwisha kamatwa,” imeeleza taarifa hiyo.
Misime ameongeza kuwa jeshi hilo linaendelea kushughulikia uhalifu wa aina hiyo, akisisitiza kuwa bado kuna watu hawajafikiwa na mkono wa sheria, lakini watachukuliwa hatua mara taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Jeshi hilo limewataka Watanzania kuendelea kutumia mitandao ya kijamii kwa njia sahihi na yenye manufaa kwa jamii, likisisitiza kwamba halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kuvunja sheria kupitia majukwaa hayo.