
Waziri Mkuu mpya wa Ufaransa, Sebastien Lecornu, amejiuzulu ikiwa ni wiki chache tu baada ya kuteuliwa kwake.
Taarifa ya kujiuzulu kwake imetolewa leo October 06, 2025 na anakuwa Waziri Mkuu wa tano wa Ufaransa katika kipindi cha chini ya miaka miwili kuchukua uamuzi huo.
Inaelezwa kwamba alikuwa na kazi nzito ya kuishawishi nchi na wawekezaji kwamba angeweza kuunganisha bunge lenye migawanyiko na kutofautiana vya kutosha ili kupitisha bajeti ya mwaka 2026.
Waziri huyo aliteuliwa mapema mwezi Septemba mwaka huu, huku kukiwa na hali ya machafuko ya umma na kutoridhika juu ya hali isiyo na mpangilio ya masuala ya taifa hilo.
Hatua ya Lecornu kujiuzulu imejiri ikiwa ni saa chache baada ya kuteua baraza lake jipya la mawaziri, ambapo nafasi nyingi muhimu ziliendelea kushikiliwa na mawaziri waliokuwepo. Kabla ya hatua ya Waziri mkuu huyo kujiuzulu, upinzani walitishia kuiangusha serikali yake, jambo linalodhihirisha ni jinsi gani kuna mzozo na mkwamo mkubwa wa kisiasa nchini Ufaransa.
Muda mfupi baada ya uamuzi huo, Ikulu ya Ufaransa imetoa taarifa ikisema kuwa Rais Macron amekubali barua ya kujiuzulu kwa Lecornu.
Siasa za Ufaransa ziliingia kwenye misukosuko tangu rais Macron alipochaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2022 na zilivurugika kabisa baada ya uchaguzi wa mapema wa Bunge wa mwaka jana ambapo hakuna chama chochote kilichofanikiwa kupata wingi unaohitajika wa wabunge.