
Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela Kijana Musa Shija (32) na kifungo cha miaka 30 jela Bi. Hollo Shija (36) kwa kosa la kuishi kama mume na mke hadi kupata Mtoto, wakati wao ni Ndugu wa damu waliotokana na Baba mmoja na Mama mmoja.
Hukumu hiyo imetolewa na hakimu Mkazi, Aziz Khamis kwa washtakiwa hao wakazi wa kijiji cha Mandang’ombe baada ya Mahakama kujiridhisha kupitia vielelezo ikiwemo vipimo vya DNA na Mashahidi 11 waliothibitisha makosa hayo.
Hakimu amesema kosa la ndugu kujamiiana ni kinyume na kifungu cha 158, cha kwanza (b) na kifungu cha 160 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 6, marejeo ya mwaka 2022, ambapo kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi Vedastus Wajanga, kati ya mwaka 2018 hadi July 30, 2024 Washtakiwa walikuwa wakiishi pamoja kama Mume na Mke na wakapata Mtoto mmoja.
Washtakiwa walifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza August 12, 2024 ambapo walikiri makosa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa Mussa na 30 na Hollo kisha wakakata rufaa Mahakama Kuu na ikaamuru kesi isikilizwe upya ambapo kesi ilianza upya Mahakama ya Maswa na May 06, 2025 walifikishwa Mahakamani na kusomewa mashtka yao na wakakana kutenda licha ya vipimo vya DNA kuonesha Mtoto wao ana uhusiano nao wa damu 99.9%.
Katika utetezi wao Mussa alidai yeye ni hatma na Horro ni Mke wake halali ambaye alimtolea mahari ya Tsh. laki 3 na elfu 25 kwa Bibi yake na Horro amedai Mussa ni Mumewe na wote wawili wamekanusha kuwa Mzee Shija Kamuga sio Baba yao Mzazi, bali ni jirani mwenye chuki dhidi ya ndoa yao lakini pamoja na utetezi wao Hakimu akawahukumu kwenda jela.