
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa endapo atapewa tena ridhaa ya kuongoza Serikali, atahakikisha anakamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka yenye urefu wa kilomita 314.
Amesema lengo ni kuufungua Mkoa wa Mwanza kwa fursa za kiuchumi na biashara.
Dkt. Samia amefafanua kuwa ujenzi wa reli hiyo umefikia asilimia 63 na utagharimu shilingi trilioni tatu, na kwamba Mkoa wa Mwanza utakuwa na vituo vitano vya abiria katika maeneo ya Mwanza mjini, Fela, Mantare na Malya.
Akinadi sera za CCM kwa wakazi wa Mwanza mjini katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Oktoba 8, 2025, katika Uwanja wa Nyamagana, Dkt. Samia amebainisha kuwa vituo hivyo vitatoa huduma mbalimbali za kiuchumi kama vile malazi, maduka, na maghala ya kuhifadhi bidhaa zitakazosafirishwa ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa vituo hivyo vitatoa fursa za kiuchumi na ajira kwa wakazi wa Mwanza, akiwahimiza kuchangamkia fursa hizo mara reli hiyo itakapokamilika.
Reli hiyo pia itaunganisha Bandari Kavu ya Fela mkoani Mwanza.
Dkt. Samia amesisitiza kuwa akipewa ridhaa ya kuongoza tena, ataendeleza mkakati wa kuiunganisha Dar es Salaam na Mwanza kupitia reli ya SGR itakayowezesha abiria na mizigo kusafiri kwa masaa nane, hatua itakayofungua zaidi fursa za biashara na uchumi nchini pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara.