
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesitisha kampeni za ubunge katika Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro, hadi maelekezo mengine yatakapotolewa kufuatia kifo cha mgombea wa CUF, Daudi Ntuyehabi.
Ntuyehabi, alifariki dunia Oktoba 7, 2025 majira ya saa 1:30 usiku, katika Kijiji cha Kilingi, Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro baada ya kushambuliwa na kundi la watu wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kwa kumchoma kwa kisu tumboni Abdul Issah Mohamed, mkazi wa eneo hilo, na kusababisha utumbo kutoka nje wakati alipokwenda kuamua ugomvi wa mgombea huyo na mtu mwingine ambaye walikuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ ya vinjwaji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jimboni humo, Marco Masue amesema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi mgombea ubunge anapofariki na ikathibitishwa na INEC shughuli za kampeni za ubunge katika jimbo hilo zinasitishwa mpaka itakapotangazwa vinginevyo.
Aidha, amesema shughuli za kampeni za urais na madiwani katika Jimbo hili zinaendelea kama kawaida.
Mapema leo Oktoba 8, 2025 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa tukio hilo la mauaji ya Ntuyehabi.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kutoa wito na kukemea tabia ya baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi kwani mara nyingi imekuwa ikisababisha madhara makubwa kama haya yaliyotokea katika tukio hilo.
Akitoa pole kwa familia ya mgombea huyo, Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Siha, Adam Ramadhan amesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mgombea huyo