
Serikali ya Mkoa wa Mwanza imesema imeweka mazingira wezeshi na shirikishi kwa wawekezaji wote wanaotamani kuwekeza katika Mkoa huo ikiwa ni sambamba na kuwahakikishia usalama wa kutosha.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda leo Oktoba 10, 2025 alipokuwa akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa ofisi za Tafiti za Jiolojia, tathmini na uchunguzi wa haki muhimu za uchimbaji madini.
Mtanda amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutunga na kuweka sera ambazo zitaruhusu Wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwa na lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amesema mahusiano na ushirikiano mwema na wa muda mrefu wa zaidi ya miaka 60 uliojengwa na nchi ya Tanzania na Jamhuri ya China umeendelea kukua na kuimarika hali inayopelekea kuongezeka kwa biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo.
“Na huu uhusiano ndio umepelekea kampuni ya Yudi kuimarisha mizizi yake kwa miaka 15 hapa Mwanza, na mimi naendelea kuwahakikishia Serikali ya Mkoa itaendelea kuwaunga mkono katika shughuli zenu muwapo hapa Mwanza”.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kuelezea kwa ufupi mafanikio ya sekta ya madini Mkoani Mwanza ambapo amesema kazi za kudumu zilizotengenezwa ni 2453 na kazi za muda ni 5986 Aidha, fursa za biashara kwa wajasiriamali wakubwa wa kati na wadogo zimekua na kufikia wastani wa thamani ya shilingi bilioni 30 kwa mwezi.
Mradi huo wa Hifadhi ya Ofisi ya Mwanza unajumuisha jumla ya eneo lililopangwa la ujenzi la takriban mita za mraba 5,000, na uwekezaji wa jumla ya takriban bilioni 8.5, ambao ukikamilika utakuwa na manufaa mbalimbali kama vile kuwa na ofisi ya Tawi la Tanzania la Kituo cha Ushirikiano wa Jiosayansi kati ya China na Afrika.