
Mahakama kuu Masijala Kuu Dodoma imesogeza mbele hukumu ya kesi ya Luhaga Mpina dhidi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na sasa itasomwa Oktoba 15, 2025.
Mwenyekiti wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo Jaji Fredrick Manyanda ametaja sababu kuu mbili zilizopelekea kuahirishwa kwa kesi hiyo ambazo kwamba majaji wanaendelea kutafakari na sababu ya pili ni kwamba wanataka kuandika vizuri hukumu ili isiwe na mashaka.
Hata hivyo, amesema hukumu hiyo itasomwa kwa njia ya mtandao siku hiyo kuanzia majira ya saa tatu asubuhi hivyo amemuagiza Msajili wa Mahakama Kuu Masijala Kuu Dodoma kuhakikisha mtandao wa Mahakama unakuwa kwenye hali nzuri ili Watanzania wasikilize.
Leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 kesi iliitwa kwa ajili ya hukumu na viongozi wa Chama Cha ACT -Wazalendo ambao ni Dorothy Semu na Kaimu Katibu Mkuu wa chama Mbarala Maharagande walifika mapema.
Wengine waliofika mapema leo ni Luhaga Mpina na Fatuma Fereji ambao ndiyo waliomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wagombea Ubunge wa chama hicho kwa mkoa wa Dodoma na Morogoro na wanachama wengi wakiwa ni vijana.
Kesi hiyo, ambayo imevuta hisia za wadau wa siasa na wanasheria nchini, inahusu hoja za kisheria kuhusu uhalali wa uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwazuia wagombea wa nafasi ya Urais wa chama hicho kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao kama wagombea.