
Kwa mara ya kwanza, wanafunzi milioni 1.6 wa darasa la nne wanatarajiwa kuanza upimaji wa kitaifa Oktoba 22, na 23 mwaka huu kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 toleo 2023 na mtaala ulioboreshwa.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 21, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said Mohamed wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Profesa Mohamed amesema wanafunzi hao watafanya mitihani ya masomo sita ambayo ni sayansi yenye hisabati, jiografia na mazingira na upande wa sanaa ni michezo, Kiswahili, Kiingereza na historia ya Tanzania na maadili.
Pia, kutakuwa na uchaguzi wa masomo matatu ambayo ni lugha ya Kichina, Kiarabu na Kifaransa.
Profesa Mohamed amesema katika takwimu hizo wanafunzi watakaofanya upimaji wa lugha ya Kiingereza ni 106,503 sawa na asilimia 6.7, lugha ya Kiswahili milioni 1.475.
Pia, amesema wanafunzi wenye mahitaji maalumu miongoni mwa wanafunzi hao ni 5,750 ambapo kati yao wenye uoni hafifu ni 1,164 na wasioona 111,wenye uziwi ni 1,161 na wenye ulemavu wa akili 1,641 na wenye ulemavu wa viungo 1,673. Profesa Mohamed amesema katika upimaji huo, masomo sita pekee ndiye yatatumika kufanyiwa upimaji baada ya kuchaguliwa na wataalamu.
aidha Profesa Mohamed amebainisha kuwa Maandalizi kwa ajili ya Upimaji wa Darasa la Nne yamekamilika, pamoja na kusambazwa kwa karatasi na nyaraka zote katika halmashauri na manispaa nchini.
Prof. Mohamed amesema wasimamizi wamepewa mafunzo ya kuhakikisha vituo vya upimaji vipo salama na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.
“Wanafunzi wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la hisabati, pia dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine, kama mwongozo wa Baraza unavyoelekeza,” ameongeza.
Pia, amesema kwamba taarifa zinazoenea hasa mitandaoni kwamba matokeo ya Darasa la Saba mwaka 2025 yametangazwa si za kweli, na iwapo yakitoka vyombo vya habari vitashirikishwa na pia matokeo hayo rasmi huwekwa kwenye tovuti ya NECTA.