Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, amesema Serikali iko mbioni kuimarisha barabara ya kilomita 38 inayounganisha Kijiji cha Rukoma na Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale Wilayani Uvinza.
Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo, Balozi Sirro amesema ubovu wa barabara umekuwa kikwazo kikubwa kwa utalii kwani Watalii hulazimika kutumia kati ya saa tano hadi sita kufika hifadhini wakitokea Kigoma mjini.
Kutokana na kadhia hiyo mkuu huyo wa mkoa wa Kigoma amesisitiza kuwa kuboresha barabara ni hatua muhimu kwa maendeleo ya utalii na uchumi wa Vijiji vinavyounganishwa na Barabara hiyo.

Naye Mkuu wa Hifadhi ya Milima ya Mahale, Kamishna Msaidizi Halid Mngofi, amebainisha kuwa idadi ya Watalii imeongezeka kutoka 210 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 923 mwaka 2023/2024 lakini hata hivyo changamoto kubwa ni ubovu wa barabara hasa nyakati za mvua ambapo watalii hulazimika kutumia Ndege, uvamizi wa hifadhi, ujangili na Wanyama wakali kushambulia Wananchi wanaoingia hifadhini kinyume na taratibu.
Hifadhi ya Milima ya Mahale inajulikana kwa idadi kubwa ya Sokwe mtu takribani 900 pamoja na Wanyama wengine kama chui, nyati, simba na mamba vilevile hifadhi hiyo pia ni kivutio cha utalii wa uvuvi wa samaki
