Rais Samia Suluhu Hassan amesema wadhifa wa uwaziri mkuu hauhitaji urafiki, undugu na jamaa, badala yake ni nafasi ya kulitumikia Taifa.
Katika maelezo yake hayo, amemwambia Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kwa umri alionao wadhifa huo ni mzigo mkubwa kwake, kwani atakumbwa na vishawishi vya ndugu, jamaa na marafiki.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Novemba 14, 2025 alipohutubia baada ya uapisho wa Waziri Mkuu, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
“Tukutakie kazi njema, mzigo huu si mdogo na kwa umri wako, sijui Kassim aliingia akiwa na umri gani, mzigo huu ni mkubwa, kwa umri wako vishawishi ni vingi vya marafiki, ndugu, jamaa na wengine.

Nafasi yako ile haina rafiki, ndugu wala jamaa ni nafasi ya kulitumikia Taifa hili,” amesema.
Aidha Rais Samia amesema uteuzi wa Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, umepitia ushindani mkubwa na vigezo kadhaa, akiwashinda wenzake kwa sifa.
Miongoni mwa sifa alizozitaja ni uzoefu wa kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa katika Wizara ya Fedha iliyomwezesha kujua chochoro zote za kupata fedha za utekelezaji wa majukumu serikalini.
“Vigezo vyote vilivyopimwa, tumepima katika maeneo mbalimbali vya kuitumikia nchi hii na kulitumikia Taifa hili.
Kubwa zaidi ni kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Rais Samia ameongeza kuwa, Dkt. Mwigulu alikuwa Waziri wa Fedha, amesema anazijua chochoro zote za kupata fedha hivyo atamsaidia atakayeteuliwa kushika wadhifa huo ili kuwezesha utekelezaji wa kazi mbalimbali za Serikali.