Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama hususani Ofisi ya DPP kuchuja makosa ya Vijana walioshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia maandamano ya October 29, 2025 na kwa wale waliofanya makosa kwa kufuata mkumbo waachiwe huru.
Akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma leo November 14, 2025 amesema anatambua kuna Vijana wengi wamekamatwa kwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya na wengine wamefuata mkumbo.
“Ninavielekeza vyombo vya sheria, hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu. Kwa wale wanaoonekana walifuata mkumbo bila dhamira ya kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao,” amesema.
Amesema wapo vijana ambao, kulingana na ushahidi wa klipu za maandamano, “walikuwa wanaimba kwa ushabiki” bila kufahamu uzito wa wanachokifanya.
Aidha Rais Dkt. Samia amesema taifa linapitia kipindi kigumu kutokana na vifo na uharibifu wa mali vilivyoripotiwa katika vurugu za siku ya uchaguzi, na kwamba hatua za msingi zimeanza kuchukuliwa ili kurejesha maelewano na amani.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa taifa halijengwi kwa ushabiki wa ghasia bali kwa umoja, maelewano na uwajibikaji akiwataka kuzingatia misingi ya amani ambayo taifa limejengwa juu yake, akiwakumbusha kuwa matendo ya hasira na fujo yanaweza kuvuruga misingi hiyo.
Aidha amewahimiza vijana kutokubali kuchochewa au kushawishiwa kuharibu taifa lao.
Moja ya hatua itakayotufikisha katika maelewano ni marekebisho ya Katiba, Serikali imeahidi kulifanyia kazi suala la mabadiliko ya Katiba ndani ya siku 100 za muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano,”- Dkt. Samia Suluhu Hassan – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imedhamiria kuanzisha Wizara itakayoshughulikia masuala ya Vijana ambapo pia amesema anatarajia kuwa na Washauri watakaomshauri kuhusu mambo ya Vijana ikiwemo changamoto zao.