Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limetoa mapendekezo mahususi ya kitaifa kwa ajili ya kuponya majeraha yaliyotokana na machafuko na maafa ya kisiasa ambayo yametajwa kuutikisa umoja wa Watanzania tangu Oktoba 29, 2025.
Akisoma tamko hilo Novemba 15, 2025, baada ya siku nne za tafakari na sala kuanzia Novemba 11 hadi 14, 2025 Rais wa Baraza hilo Askofu Wolfgang Pisa, amesema taifa limeumizwa na liko katika hatari ya kugawanyika zaidi, hivyo ni muhimu kwa viongozi na mamlaka husika kuchukua hatua hizi ili kurejesha matumaini, haki na amani.
Maaskofu wamesema viongozi na mamlaka lazima walipe umuhimu tukio hilo la maafa, wakiri ukweli, watoe pole kwa familia na kukemea mauaji yaliyofanyika wakisisitiza kuwa “waliouawa ni ndugu zetu.”
Baraza linataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibishwe au wawajibike, kwani hasira kubwa ya wananchi inatokana na kuona hakuna anayechukuliwa hatua licha ya raia kuumizwa au kupoteza maisha.
Maaskofu wanapendekeza uchunguzi wa kina usiofungamana na upande wowote, ukihusisha taasisi za kimataifa, dini, wataalamu wa demokrasia, asasi za kiraia, na serikali kuwa tayari kupokea matokeo na kuyafanyia kazi, wanahimiza viongozi wote waishi kwa uadilifu, ukweli na uwajibikaji na wanataka wote waliokamatwa kabla, wakati au baada ya uchaguzi kwa hila na bila mashauri ya haki waachiwe huru bila masharti.
Aidha TEC wametaka mchakato wa Katiba mpya uanze mara moja kwa kushirikisha wadau wote ili taifa lisirudi kwenye machafuko.
Pia TEC imewaalika Watanzania kuendelea kusali ili haki, amani, ukweli na uponyaji viweze kurejea, huku ikiwafariji waliopoteza wapendwa na kuwaombea majeruhi wapone.