Taarifa mpya kutoka kwa familia ya marehemu Emmanuel Mathias, maarufu kama MC Pilipili, zimezua maswali mazito kuhusu mazingira ya kifo chake. Akizungumza na vyombo vya habari, msemaji wa familia, Paschal Maingu, amesema taarifa walizopokea kutoka kwa ndugu wa karibu zinaonesha kuwa MC Pilipili alifariki katika hali ya mateso makubwa.
Kwa mujibu wa Maingu, mdogo wa mwisho wa marehemu ndiye aliyetoa taarifa hizo za awali, akisema mwili wa Pilipili ulikutwa na majeraha, jambo linaloibua hisia kuwa huenda alifanyiwa ukatili kabla ya mauti kumkuta.
Familia inaendelea kusubiri taarifa rasmi kutoka kwa polisi ili kufahamu ukweli kamili wa kilichotokea kabla ya kupanga utaratibu wa mazishi. Kwa sasa, Maingu amesisitiza kuwa familia imeingia katika majonzi makubwa kutokana na mazingira tata yanayozunguka kifo cha mpendwa wao.
Kifo cha MC Pilipili, mmoja wa wacheshi walioleta furaha kwa Watanzania kwa miaka mingi, kimeacha simanzi na maswali mengi miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani. Wengi wanaitazama taarifa ya familia kama hatua ya kwanza kuelekea kupata majibu kuhusu kilichosababisha kifo chake.
Mashabiki na wasanii mbalimbali wanaendelea kutoa pole na dua kwa familia ya marehemu, wakimtaka Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi