Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amewataka Wataalamu wa Takwimu nchini kuchakata kwa weledi na kutoa takwimu na taarifa sahihi kwa jamii ili kuwapa mwelekeo wa shughuli za kufanya kwa wakati fulani ili kupata maendeleo.
Mtanda ametoa wito huo leo tarehe 18 Novemba, 2025 wakati akizungumza na wataalamu wa Takwimu kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa waliokutana kwenye maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika.
Amesema wananchi wanapanga maisha yao kiuchumi na kijamii kwa kutegemea taarifa sahihi kutoka serikalini mathalani kuhusu bei za bidhaa au hali ya upatikanaji wa pembejeo hivyo wanawategemea kuwapatia taarifa sahihi za namna gani waenende.
“Mipango, taarifa na takwimu sahihi ndizo zinazotuwezesha kufanya makadirio ya maisha ya baadaye hivyo basi ninyi ndio wataalamu mnaotegemewa kufanya utafiti na kutumia ubunifu wa kuchakata na kutoa taarifa sahihi kwao ili kuwapa mwelekeo hivyo siku zote lazima muzingatie hilo.”
Ameongeza kuwa Dira ya taifa ya maendeleo kwa 2025/2050 inawategemea wataalamu hao katika kuweka misingi na mikakati ya uwekezaji na uwajibikaji katika kwenye kila sekta hivyo takwimu zina faida kubwa kwenye kupanga mifumo ya maamuzi sahihi ya maendeleo.

“Pamoja na kwamba takwimu zinasaidia kuweka misingi sahihi katika kupanga maendeleo zinasaidia pia kukuza utafiti na uvumbuzi, kuimarisha uchumi na uwekezaji, kuweka taswira ya ukweli, kuboresha huduma za jamii pamoja na kuboresha ufanisi na kupunguza hasara” Amesisitiza RC Mtanda.
Aidha, amewapongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kutekeleza kwa ufanisi jukumu kubwa la Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika kwa mafanikio mwaka 2022 nchini na ametoa wito kwa wananchi kusoma taarifa za tume hizo katika tovuti na mbao za matangazo ili kupata taarifa sahihi za mambo mbalimbali.

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika ambayo yameanza rasmi mwaka 1990 baada ya mkutano wa Mawaziri wa Uchumi na Mipango wa nchi za Afrika (Addis Ababa) kwa mwaka 2025 yanachagizwa na kaulimbiu ya ‘Kuongeza Ubunifu katika Matumizi ya Takwinu na Taarifa ili kujenga Jamii Jumuishi.’