Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameagiza kurejeshwa kwa huduma ya mabasi ya mwendokasi kituo cha Mbagala kuanzia Novemba 20, 2025, ikiwa ni hatua za awali za serikali kuchukuliwa baada ya vurugu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua baadhi ya vituo vilivyoharibiwa katika Wilaya ya Temeke, Chalamila alisema serikali ina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kuchelewa, hasa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kama Mbagala.
Agizo hilo linakuja baada ya ombi la Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, ambaye aliomba baadhi ya huduma muhimu, zikiwemo za usafiri wa mwendokasi, kurejeshwa ili kupunguza usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.
Bw Chalamila ameeleza kuwa licha ya uharibifu mkubwa wa vituo vya mwendokasi, hakuna shule yoyote iliyoripotiwa kuchomwa au kuharibiwa wakati wa Vurugu hizo.

RC Chalamila Amesisitiza kuwa serikali itaendelea na tathmini ya uharibifu wa mali za umma na watu binafsi ili kuweka mkakati madhubuti wa urejeshaji wa huduma hizo.
Chalamila pia ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa watulivu na kudumisha amani, mshikamano na upendo katika maeneo yao na kuepuka kujiingiza katika Vurugu zinazo hatarisha amai.